Ndg.
Fadhili Fabian Ngajilo alikuwa akiwasilisha ripoti ya kuboresha muundo
wa UVCCM mwezi Juni, 2012 ndani ya ukumbi wa NEC-CCM katika jengo la
White House Makao Makuu ya CCM, Dodoma.
YAH:
NDG. FADHILI FABIAN NGAJILO
KUGOMBEA NAFASI YA MWENYEKITI WA CCM MKOA WA IRINGA
Kutokana na uchaguzi unaoendelea ndani ya Chama cha Mapinduzi, Mimi Fadhili Fabian Ngajilo (pichani) ambaye ni Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Iringa nitakayestaafu mwezi wa Oktoba kutokana na umri wangu kuvuka ukomo wa kikanuni wa miaka 30, sasa ninagombea nafasi ya Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa,
nimechukua fomu tarehe 26 Julai 2011. Ninagombea nafasi hii kwa kuwa
nimejipima, nimejichunguza na kuona kuwa nafasi hiyo ninaimudu.
Ninauzoefu na shughuli za chama kupitia idara nilizoziongoza kama Umoja
wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Ujumbe wa Kamati ya Siasa ya
CCM Mkoa na Halmashauri Kuu ya CCM ya Mkoa wa Iringa, Mjumbe Mkutano
Mkuu wa CCM Taifa na Baraza Kuu la Taifa la Umoja wa Vijana wa CCM.
Lakini pia ukitazama Wasifu wangu utagundua kuwa mimi nimeanzia ngazi ya
chini (mtaa) kuwa kiongozi, nimepanda taratibu hadi mkoani. Nina
malengo kadhaa endapo nitafanikiwa kuwa Mwenyekiti wa Chama cha
Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa, mimi ninaamini kuwa ‘Fikra sahihi na uchumi bora wa chama utaifanya CCM kuwa imara zaidi na kuendelea kushika dola’ kwa hiyo hii ndio itakuwa kauli mbiu itakayoongoza chama mkoa wa Iringa kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, malengo mengine ni;
1. Kama
nilivyoonyesha awali kuwa lengo kuu la kuwania nafasi hii ni kuujenga
uchumi wa chama katika ngazi za kata na matawi ya chama. Tutaanzisha
kampuni ya kibiashara itakayoendeshwa na wataalamu na itajikita katika
kubuni, kuanzisha na kusimamia miradi mbalimbali ambayo itamilikiwa na
kata na matawi yote ya CCM Mkoa wa Iringa. Tutatoa kipaumbele kwenye
miradi ya Kilimo, Misitu, Majengo na Usafirishaji.
2. Nitasimamia
mshikamano wa wanachama na viongozi wa CCM Mkoa wa Iringa. Njia kuu ya
kutekeleza hili ni kwa kutenda haki kupitia vikao vya maadili vya chama
vya ngazi zote. Kwa hiyo tutahimiza ngazi zote kufanya vikao vingi kwani
ndio nguzo muhimu ya uimara wa chama.
3. Nitahakikisha
Chama cha Mapinduzi (CCM) kinaendelea kushika dola, hakuna jimbo la
uchaguzi litakaloenda upinzani chini ya uongozi wangu. Njia ya
kufanikisha hili ni kwa kuisimamia Serikali kupitia Halmashauri za
Wilaya katika kutekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM. Nitaongeza nguvu
kwenye kuziba mianya ya ufisadi dhidi ya mali za umma katika Halmashauri
zetu na kuhakikisha fedha zinazotengwa kwa kazi za maendeleo inafanya
hivyo.
4. Nitaimarisha
idara za Itikadi na Uenezi, Fedha na Uchumi, Umoja wa Wanawake (UWT),
Umoja wa Vijana (UVCCM) na Jumuiya ya Wazazi mkoa wa Iringa. Vyombo hivi
vitaimarishwa kwa kupewa watendaji wenye weledi, vifaa na kuimarisha
uchumi kupitia miradi yake. Makambi ya kuwaandaa makada kiitikadi na
kisiasa yatafanyika kupitia programu maalumu itakayoanzishwa na
kusimamiwa katika Chuo cha Ihemi, mpango huu utaitwa ‘CCM Vital Program’
kwa kifupi CCMVP. Mpango huu utaandaa makada wakufunzi, Utaanzisha
madarasa ya Itikadi ngazi za Matawi na Kata, utaandaa vitabu na vijarida
vya kujisomea masuala mbalimbali ya chama.
5. Tutawaenzi
wazee kwa kuwaanzishia Umoja wao (Umoja wa Wazee wa Chama cha
Mapinduzi) utakaokuwa na jukumu la kutoa ushauri kwa chama, tutaanzisha
Umoja huu katika ngazi za wilaya zote za mkoa wa Iringa. Wazee watakuwa
wakikutana katika mabaraza yao kila mara, wataanzisha shughuli za
michezo na jadi za wazee, ujasiriamali nakadhalika.
6. Nitaamsha
ari mpya kwa wanachama wa CCM Mkoa wa Iringa ili wajisikie na kujivunia
uimara wa chama chao. Tutafanya hivyo kwa kusimamia maamuzi na fikra
sahihi na za kisasa ndani ya chama. Tutafanya mikutano ya kuhamasisha
maendeleo, na kujibu hoja na propaganda chafu za upinzani dhidi ya CCM.
7. CCM
Mkoa wa Iringa itajishughulisha na shughuli za kijamii wakati wa
uongozi wangu ikiwamo Michezo kwa vijana, maveterani, wanawake na wazee.
Kundi la vijana litapewa kipaumbele katika kuhamasisha utengenezaji wa
fursa za ajira. Lakini pia Mkoa utajishughulisha na kuhamasisha shughuli
za ujasiriamali na biashara katika sekta zote.
WASIFU WANGU(CV)
(a) KUZALIWA NA KAZI
Mimi ni kijana niliyezaliwa tarehe 27 Juni, 1979 Manispaa ya Iringa. Kwa sasa mimi ni Mhadhiri
Chuo Kikuu cha St. John’s University. Lakini pia nimeshawahi kuwa
Mwendeshaji wa Semina (Seminar Leader) katika Chuo Kikuu cha Dar es
salaam.
(b)ELIMU NA MAFUNZO YA SIASA
Nimesoma
Shule ya Msingi ya Mapinduzi na Chemchem zote zikiwa Manispaa ya
Iringa, Baadae mwaka 1995 nilijiunga Shule ya Sekondari ya Lugalo ya
Manispaa ya Iringa kwa ajili ya kidato cha I-IV, na mwaka 1999
nilijiunga na Shule ya Sekondari ya Makongo JWTZ iliyopo Dar es Salaam
kwa ajili ya kidato cha V na VI. Kati ya mwaka 2003-2006 nilisoma
Shahada ya Historia na Mambo ya Kale (B.A. History and Archaeology) ya
Chuo Kikuu cha Dar es salaam, mwaka 2006 nilichaguliwa kusoma Shahada ya
Historia katika fani za Siasa na uchumi (M.A History) katika Chuo Kikuu
cha Dar es salaam. Kwa sasa naandika andiko linalohusu ajira za watoto
kwa ajili ya Shahada ya Udaktari wa Falsafa (Ph.D). Pia mimi ni mtaalamu
wa masuala ya kompyuta mwenye cheti cha Computer
Literacy Certificate kutoka Chuo cha Compware College. Pamoja na yote
hapo juu nimefanya tafiti mbalimbali za kitaaluma.
Nimehudhuria
mafunzo na kambi mbalimbali za siasa zikiwemo zilizoandaliwa na Taasisi
ya Ujerumani ya Friedrich Ebert Stiftung (FES) mwaka 2009. Pia Mimi ni
mkufunzi wa Siasa na Itikadi kupitia mafunzo (TOT) ambayo niliyapata
mwaka 2010 chini ya Mzee Kingunge Ngombalemwiru.
(c) UZOEFU KATIKA UONGOZI
§ Kwa sasa ni Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Iringa, ambaye ninastaafu mwezi wa Oktoba mwaka 2012.
§ Pia mimi ni Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Tanzania, ambaye pia ninastaafu nafasi hiyo mwezi Oktoba.
§ Nilikuwa Mjumbe wa Kamati Maalumu ya Baraza Kuu la UVCCM Taifa ya kuboresha Muundo na Madhumuni ya Umoja huo, kamati ambayo imezunguka nchi nzima kukusanya maoni ya wanachama.
§ Mwaka 2010 niliwania nafasi ya kugombea Ubunge kupitia kura za maoni katika Jimbo la Iringa Mjini. Lakini kura hazikutosha.
§ Kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita nimekuwa Mjumbe wa Kamati ya Siasa na Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Iringa.
§ Kabla
ya mwaka 2008 nilitumikia chama kwa kuwa Mjumbe wa Baraza la Vijana wa
Chama cha Mapinduzi Manispaa ya Iringa. Nilikaimu uenyekiti wa UVCCM wa
kata ya Kwakilosa, Manispaa ya Iringa, ambako pia nilikuwa Meneja
kampeni wa kata uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.
§ Nilikuwa
Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Jangwani, Kata ya Kwakilosa, Manispaa ya
Iringa kati ya mwaka 2009 hadi 2004. Hii inaonyesha kuwa nimeanza
uongozi kuanzia ngazi ya chini kabisa.
§ Nikiwa
nasoma Chuo Kikuu cha Dar es salaam, nilikuwa Mwenyekiti wa Wanafunzi
kupitia taasisi ya ‘Iringa University Students Association’ (IRUSA)
§ Lakini
pia nilipokuwa nasoma Shule ya Sekondari ya Makongo High School
nilikuwa Mwenyekiti wa wanafunzi kupitia umoja wao uitwao ‘Tanzania
Youth Catholic Student’s Society (TYCS)’
Kauli Mbiu yangu
‘Fikra sahihi na uchumi bora wa chama utaifanya CCM kuwa imara zaidi
na kuendelea kushika dola’
Kidumu Chama Cha Mapinduzi!
SIMU YANGU: 0767-609477
No comments:
Post a Comment